Jaymo Ule Msee atangaza ujio wa kipindi chake

Anapanga uzinduzi rasmi Novemba 9, 2026.

Marion Bosire
1 Min Read

Mtayarishaji wa maudhui nchini Kenya, Jaymo Ule Msee, ametangaza ujio wa kipindi chake chenye matoleo 20 chenye jina, “Inside the Life of a Prodigal Creator”.

Anapanga uzinduzi rasmi Novemba 9, 2026.

Katika ujumbe aliochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Jaymo, ambaye jina lake halisi ni Wilson Muirani Gathoni, alisema kipindi hicho kitajikita katika uzoefu wake binafsi, kama kuhusika kwake na siasa, changamoto za kifedha na juhudi za kufufua taaluma yake ya ubunifu.

Alikiri kuwa maamuzi yake ya kisiasa pamoja na makosa ya kifedha yamemgharimu pakubwa na kumwacha katika hali ngumu ya kifedha.

Pia aliomba msamaha kwa kizazi cha Gen Z kutokana na matamshi yasiyo na hisia aliyotoa Juni 25, 2025, pamoja na mashabiki walioathiriwa na maudhui yake ya kisiasa.

Jaymo alisema kipindi hicho kitakuwa na visa vya kweli kutoka kwa maisha yake, kikichanganya maigizo, vichekesho, ukweli usiopendeza na mafunzo kuhusu fedha, majivuno na ushawishi.

Aidha, aliwaomba mashabiki kumchangia kwa hiari ili kumsaidia kurejesha hali yake ya kifedha na kufufua kazi yake ya ubunifu, huku akiwahimiza wasioweza kuchangia kuunga mkono mradi huo kwa kutazama na kusambaza vipindi hivyo.

Share This Article