Washukiwa watatu wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa Nairobi

Tom Mathinji
1 Min Read

Washukiwa watatu wa ulanguzi wa Mihadarati wamekamatwa baada ya kupatikana na vipande 1,002 vya bangi katika mtaa wa Jericho Jijini Nairobi.

Kulingana na Halmashauri ya kupambana na Pombe na Mihadarati (NACADA), maafisa wa Kukabiliana na Mihadarati walivamia nyumba moja katika mtaa wa Buruburu Ijumaa alasiri baada ya kupokea habari za kijasusi.

Baada ya kupekua nyumba hiyo, maafisa hao walipata vipande 936 zinazoshukiwa kuwa bangi  na bidhaa zingine 66 za rangi nyekundu zikiwa zimefungwa kwa mifuko ya plastiki.

Watu watatu waliopatikana katika nyumba hiyo walikamatwa na wanazuiliwa katika Kituo cha polisi cha Jogoo road, wakisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa alisema operesheni hiyo ni sehemu ya juhudi za kusambaratisha ulanguzi wa Mihadarati katika maeneo ya wakazi.

Aliwapongeza wakazi kwa kutoa habari ambazo zilifanikisha kukamatwa kwa washukiwa hao.

Share This Article