Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, amesema Kenya na Urusi zinalenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kupitia pendekezo la kuunda tume ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi, itakayojukumiwa kufanikisha upanuzi wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza Ijumaa aliposhiriki mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Urusi Maxim Reshetnikov, kuhusu makubaliano hayo yaliyopendekezwa, Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alisema kuwa tume hiyo itatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu za kiuchumi, huku ikitoa nafasi mpya kwa wafanyabiashara wa Kenya na viwanda.
” Urafiki dhabiti wa kimataifa unapaswa kubuni uchumi imara, ustawi wa biashara na kubuni nafasi zaidi za kazi. Kenya inapeleka uhusiano wake na Urusi katika kiwango kingine,” alisema Mudavadi.
Tume hiyo inayopendekezwa itaongozwa kwa pamoja na wawakilishi wa ngazi ya juu wa serikali kutoka Kenya na Urusi, huku kila upande ukichagua wajumbe wake.