Raia wa Serbia wanapiga kura leo katika uchaguzi wa bunge ambapo vuguvugu la wanafunzi linalenga kumng’atua madarakani kiongozi wa muda mrefu Aleksandar Vučić, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwongo mmoja.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya maandamano ya karibu miaka miwili yaliyotokana na madai ya ufisadi na ongezeko la utawala wa kimabavu.
Maandamano yalianza mwaka 2024 baada ya watu 16 kufariki kufuatia kuporomoka kwa paa la kituo cha treni katika mji wa Novi Sad.
Vuguvugu la wanafunzi limepata uungwaji mkono wa kiwango kikubwa, likilenga kupambana na ufisadi na kuboresha elimu. Lina wagombea 250, wakiwemo maprofesa, waigizaji na wakulima, chini ya uongozi wa daktari bingwa wa moyo Ilija Srdanovic.
Hata hivyo, Vučić anasalia kuwa mpinzani mwenye nguvu, huku akiahidi kuongeza pensheni, mishahara ya wafanyakazi wa umma na kuwekeza katika huduma za afya. Wafuasi wake wanamsifu kwa kuimarisha uchumi na kuendeleza miundombinu.
Utafiti wa Ipsos uliochapishwa Alhamisi unaonyesha chama chake kinatarajiwa kupata asilimia 47 ya kura, dhidi ya asilimia 40 za wanafunzi, ingawa tafiti nyingine zinaonyesha wanafunzi wakiongoza.
Takribani wafuasi 150,000 wa vuguvugu hilo walikusanyika Belgrade Alhamisi.
Wakati huo huo, uhusiano wa Serbia na Umoja wa Ulaya umeendelea kudorora kutokana na ukosefu wa mageuzi ya mahakama, utawala wa sheria na kupambana na ufisadi.
Vučić amekanusha madai ya ufisadi na ukandamizaji, huku akidai wanafunzi wanafadhiliwa na mawakala wa kigeni, madai ambayo wameyakanusha.