Mvua kubwa inayoandamana,joto jingi na upepo mkali vinatarajiwa kushuhudiwa katika maeneo mengi humu nchini kati ya leo Jumamosi Oktoba 24 na tarehe 30 mwezi huu.
Kulingana na taarifa ya kutoka idara ya utabiri wa hewa, wakazi wa maeneo hayo yaliyobainishwa wametakiwa kuchukua tahadhari kubwa.
Mvua ya wastani wa milimita 20 inatarajiwa kushuhudiwa katika ukanda wa Pwani,Kaskazini Mashariki,Magharibi mwa nyanda za juu,Mashariki mwa Bonde la Ufa,nyanda za kati ikiwemo maeneo ya kaunti ya Nairobi na Kusini Mashariki mwa nyanda za chini.
Mvua hiyo itaandamana na upepo mkali huku maeneo ya kaskazini mwa nchini yakitarajia kushuhudia joto jingi.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa imewataka raia kuwa waangalifu dhidi ya mafuriko ambayo yatasababishwa na mvua hiyo kubwa .