Kenya kushuhudia mvua kubwa, upepo mkali kuanzia Jumamosi

Utabiri huo pia unaashiria kwamba hali ya juu ya joto itashuhudiwa katika sehemu kadhaa za nchi, hususan Kaskazini mwa nchi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mvua kubwa, upepo mkali kushuhudiwa kuanzia Jumamosi.

Halmashauri ya Huduma za Utabiri wa Hali ya Hewa (KMSA), imesema sehemu kadhaa za taifa hili zitashuhudia mvua kubwa, upepo mkali na joto jingi, ikiwtaka wananchi kuchukua tahadhari.

Kulingana na halmashauri hiyo, mvua ya zaidi ya milimita 20 katika muda wa saa 24, inatarajiwa katika kaunti za Pwani, Kaskazini Magharibi, Bonde la Ufa, Katikati ya Nchi na sehemu kadhaa za Nairobi.

“Mvua hiyo inatarajiwa kufika kilele kati ya tarehe 26 na 28 mwezi Oktoba, ikitarajiwa kupungua Oktoba 30,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Huduma za Utabiri wa Hali ya Hewa  Edward Muriuki.

Wakati huo huo, Muriuki alionya kuwa mvua hiyo itaandamana na upepo mkali utakaovuma katika maeneo ya Pwani, Mashariki na Kaskazini ya nchi.

Kwa mujibu wa KMSA,  kaunti 46 zitapokea mvua kupita kiasi.

Utabiri huo pia unaashiria kwamba hali ya juu ya joto itashuhudiwa katika sehemu kadhaa za nchi, hususan Kaskazini mwa nchi.

Share This Article