Mtu mmoja aokolewa kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka Eastleigh

Serikali ya kaunti ya Nairobi imesema jengo hilo lilikuwa bado linaendelea kujengwa lilipoporomoka, ingawa orofa ya chini ilikuwa tayari na wapangaji.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mtu mmoja aokolewa kwenye jengo lililoporomoka Eastleigh.

Huduma ya Taifa ya Polisi, imesema  mtu mmoja ameokolewa kutoka kwa vifusi vya jengo lililoporomoka katika eneo la Eastleigh, Nairobi, huku makundi ya uokoaji yakiendelea kuwatafuta watu wanaohofiwa kukwama.

Kulingana nahuduma hiyo, mtu huyo amepelekwa hospitalini kwa matibabu, huku  shughuli za uokoaji katika eneo la tukio hilo zikiendelea.

Shirika la Msalaba Mwekundu, limesema maafisa wake wanashirikiana na wale wa asasi mbali mbali kuwatafuta manusura, huku wakitoa wito kwa wananchi kuondoka katika eneo hilo.

Alipotembelea eneo hilo, Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, alisema makundi ya uokoaji yanaondoa vifusi kwa uangalifu ili kuruhusu hewa ya oksijeni kuingia ndani ya jengo hilo na kuongeza uwezekano wa kuwaokoa watu ambao bado wamekwama.

Kulingana na Sakaja, jengo hilo lilikuwa limekiuka kanuni za ujenzi na akaahidi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mmiliki wake.

Serikali ya kaunti ya Nairobi imesema jengo hilo lilikuwa bado linaendelea kujengwa lilipoporomoka, ingawa orofa ya chini ilikuwa tayari na wapangaji.

Idadi ya watu wanaohofiwa kukwama chini ya vifusi pamoja na chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo bado haijathibitishwa.

Share This Article