Rais William Ruto amesema serikali inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya afya, huku idadi ya Wakenya wanaonufaika na Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA), ikifika milioni 33.
Kulingana na Rais Ruto, idadi hiyo inaashiria hatua kubwa iliyopigwa katika sekta ya afya, tangu utawala wake ulipochukua hatamu ya uongozi wa taifa hili mwaka 2022.
“NHIF ilikuwa inahudumia idadi fulani ya watu; SHA inahudumia kila mtu. NHIF ilihudumia watu wachache waliobahatika; SHA inahudumia kila Mkenya. NHIF ilifadhili hospitali chache zilizochaguliwa, SHA inafadhili vituo vyote vya kutoa huduma ya afya kote nchini, ikiwemo vituo vya afya, na zahanati,” alisema Rais Ruto.
Akihutubia taifa wakati wa maadhimisho ya 63 ya Siku Kuu ya Mashujaa katika kaunti ya Uasin Gishu, kiongozi wa taifa alisema kupitia halmashauri ya SHA, zaidi ya vituo 10,000 vya huduma za afya vinapokea fedha moja kwa moja, vinanunua dawa, vifaa na bidhaa nyingine muhimu kulingana na mahitaji yao.
“Tangu tarehe 1 Januari mwaka huu pekee, SHA imetoa shilingi bilioni 107 kwa vituo vya afya kote nchini,” alidokeza Rais Ruto.
Alisema serikali imekumbatia mfumo wa dijitali katika utoaji wa huduma za afya, hatua aliyodokeza imerahisisha kusambazwa kwa taarifa za mgonjwa katika vituo vyote vya afya.
“Hii ni Huduma ya Afya ya Usawa. Sio huduma ya afya kwa wachache waliobahatika, lakini huduma bora ya afya kwa kila Mkenya, popote anapoishi na bila kujali hali zao,” alisema Rais Ruto.
Sherehe za Mashujaa za mwaka huu ziliandaliwa kwa pamoja na kaunti tatu za Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet na Nandi.