Ufaransa imeweka amri ya kutotoka nje wakati wa usiku katika baadhi ya maeneo ya Paris ya kati na majiji mengine, kama hatua ya kukabiliana na visa vya uporaji na misururu ghasia iliyotokea kote nchini humo.
Maafisa wa Polisi jijini Paris, walisema amri hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia saa tano usiku hadi saa kumi na mbili alfajiri katika eneo la Place de la République, ambako waandamanaji walikusanyika mwishoni mwa juma pamoja na kwenye kituo cha biashara cha Les Halles.
Wakati huo huo, serikali imepiga marufuku mikusanyiko ya umma ambayo haijaidhinishwa kwa lengo la kudhibiti mikusanyiko ya vijana katika maeneo ya Marseille, Bordeaux, Nice, Lyon , Lille pamoja na miji mingine iliyoko kaskazini mwa Ufaransa.
Siku ya Jumatatu, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, alikataa barua ya kujiuzulu kwa waziri wa usalama wa ndani Laurent Nuñez, kufuatia maaandamano ya kitaifa ya wiki jana nchini humo kupinga gharama ya juu ya maisha.
Zaidi ya watu nusu milioni walijitokeza katika barabara za miji kadhaa ya Ufaransa Jumamosi iliyopita kulalamikia gharama ya juu ya maisha.
Maandamano hayo yalisababisha uharibifu mkubwa wa mali huku magari na majumba kadhaa ya kibiashara yakiteketezwa na maduka yakiporwa.
Waziri wa usalama wa kitaifa wa Ufaransa Laurent Nuñez, alikuwa ameandika barua ya kujiuzulu mapema Jumatatu.