Rais William Ruto leo Jumanne, ataongoza taifa kuadhimisha sherehe za Mashujaa katika uwanja wa Kipchoge Keino mjini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu.
Sherehe hizo kwa mara ya kwanza zinaandaliwa kwa ushirikiano wa kaunti tatu ambazo ni Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet na Nandi, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa sherehe hizo kuandaliwa na kaunti tatu.
Kauli mbiu ya sherehe za mwaka huu ni “Ngao Yetu, Ustawi Michezoni na Uchumi Bora”.
Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, awali alitaja hatua ya kuandaa sherehe hizo katika eneo hilo, kuwa fursa bora ya kuonyesha hatua za maendeleo zilizopigwa na uwezo wake wa kiuchumi.
“Tutashirikiana na wadau wote kuhakikisha sherehe za mwaka huu za Mashujaa zinafaulu na kuashiria moyo ya umoja wa taifa hili,” alisema Gavana Bii.
Sherehe hizo zinajiri baada ya siku kadhaa za mashindano ya michezo na shughuli za kijamii katika kaunti hizo tatu. Kaunti ya Elgeyo Marakwet iliandaa mashindano ya riadha, kaunti ya Nandi ikiandaa mashindano ya Voliboli nayo Uasin Gishu ikiandaa mashindano ya soka.
Sherehe za leo ambazo ni za 63, huandaliwa kila mwaka kuwakumbuka wale waliopigania ukombozi wa taifa hili kutoka kwa wakoloni, na wale ambao michango yao imefanikisha pakubwa ustawi wa taifa hili.