Mzunguko wa wakongwe wa muziki wa Bongo Fleva unaendelea nchini Tanzania wanapoendelea kuadhimisha miaka 30 ya muziki huo, huku kamati ya maandalizi ikitaja kituo kitakachofuata.
Katika taarifa kwa umaa, kamati hiyo ilielezea kwamba maadhimisho hayo yanahamia jijini Mbeya Novemba 7, 2026, baada ya kufanyika kwa mafanikio Zanzibar, Oktoba 17, 2026.
Kamati hiyo ya maandalizi ya maadhimisho hayo imewashukuru wadhamini, washiriki na wadau mbalimbali waliochangia kufanikisha tamasha iliyofanyika Zanzibar, ikieleza kuwa mchango wao umekuwa muhimu katika kuendeleza historia ya muziki huo nchini Tanzania.
Katika taarifa aliyotoa kwa niaba ya kamati, Hamadi Ally Seneda alitaja taasisi kadhaa zilizofanikisha hafla ya Zanzibar kama benki ya Azania, mashirika ya habari ya Azam na Millard Ayo.
Seneda amesema maadhimisho hayo yanalenga kuwaenzi waanzilishi wa Bongo Fleva, kuhifadhi historia ya muziki huo na kuimarisha ustawi wa watengenezaji na waandaaji wa muziki.
Aidha, maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha jamii kutambua thamani ya kitamaduni na kiuchumi ya ubunifu wa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.
Mzunguko huu umetoa fursa wa wadau wa muziki huo na mashabiki kukutana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, kufurahia na kutafakari safari ya miongo mitatu ya Bongo Fleva na mchango wake katika tasnia ya burudani na uchumi wa ubunifu.