Nandy afunguka kuhusu changamoto za kuandaa 911

Alifichua kuwa wakati mwingine alikuwa akilia peke yake usiku na kujiuliza iwapo angefanikiwa kutimiza ndoto yake.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Faustina Mfinanga maarufu kama Nandy amefunguka kuhusu changamoto alizopitia wakati wa utayarishaji wa albamu yake mpya ya “911”.

Ameelezea kwamba safari hiyo ilihusisha kazi nyingi, kujitolea na nyakati ngumu za kihisia.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nandy alisema alitumia muda mwingi akikesha na timu yake kujadili mawazo, kuandika mistari ya nyimbo na kufanya marekebisho ili kuhakikisha albamu hiyo inakuwa bora.

Msanii huyo alifichua kuwa wakati mwingine alikuwa akilia akiwa peke yake usiku na kujiuliza iwapo angefanikiwa kutimiza ndoto yake, lakini upendo na uungwaji mkono wa mashabiki wake vilimpa nguvu ya kuendelea.

Nandy pia alimshukuru Mungu, akiwataja mashabiki wake kama familia na chanzo kikubwa cha motisha katika safari yake ya muziki.

Alisema albamu hiyo ameitengeneza kwa moyo wake wote, akilenga kuwagusa mashabiki, kuwaburudisha na kuwapa muziki wanaoustahili.

Kazi hiyo ya “911” inatarajiwa kutolewa Novemba 27, 2026, kupitia majukwaa yote ya kidijitali.

Albamu hiyo inayotarajiwa ina jumla ya nyimbo 16 zinazojumuisha alizoimba peke yake na alizoshirikisha wasanii wengine kama Nyashinski wa Kenya, Sheebah Karungi wa Uganda, Tiwa Savage wa Nigeria na Ferre Gola wa DRC kati ya wengine.

Alihusisha watayarishaji muziki 6 ambao ni S2Kizzy, Kimambo, Beats by Timmy, Banginbeats, Trone na Ammy Wave.

Share This Article