Chagga akanusha madai ya kufurushwa Uingereza

Amesisitiza kuwa bado ana uhuru wa kurejea nchini humo na kuendelea na kazi zake.

Marion Bosire
1 Min Read

Geoffrey Kyagambiddwa, ambaye alikuwa meneja wa wasanii na mwimbaji nchini Uganda maarufu kwa jina la Chagga, amekanusha madai kwamba alifukuzwa nchini Uingereza.

Amesisitiza kuwa bado ana uhuru wa kurejea nchini humo na kuendelea na kazi zake.

Chagga alisema alikuwa akifanya kazi jijini London kabla ya kurejea Uganda, akisisitiza kuwa kurejea kwake hakukutokana na kufukuzwa nchini Uingereza.

“Nilikuwa nikifanya kazi London, Uingereza, na bado nitarudi kuendelea kufanya kazi,” alisema, huku akihoji ni kwa namna gani watu waliafikia hitimisho kwamba alikuwa amefukuzwa.

Alieleza kuwa maisha yake nchini Uingereza yalikuwa na changamoto, akisema baadhi ya watu aliowaamini hatimaye walimgeuka. Pia alionyesha kukatishwa tamaa na watu aliotarajia wampokee katika uwanja wa ndege lakini hawakufika.

Chagga alidai zaidi kuwa baadhi ya washirika wake walitaka ajisalimishe kwa polisi wa Uingereza kama sehemu ya mchakato unaohusiana na kuomba hifadhi, lakini akasema hilo halikuwa katika mipango yake.

Kwa mujibu wa mwimbaji huyo, maisha yake London yalikuwa na watu wema na wabaya, sawa na hali ilivyo Kampala.

Licha ya changamoto alizokumbana nazo, Chagga amesisitiza kuwa anakusudia kurejea Uingereza na kuendelea na kazi zake, akipuuza uvumi unaohusiana na kuondoka kwake nchini humo.

Share This Article