Evelyn Wanjiru aelezea safari yake ya subira katika kitabu ‘The Wait’

Kitabu hicho kinalenga kuwatia moyo watu binafsi na wanandoa wanaopitia changamoto kama alizopitia.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya, Evelyn Wanjiru, amezindua kitabu kiitwacho “The Wait” ambacho kwa kiwango kikubwa ni simulizi kuhusu safari yake ya subira.

Ikumbukwe kwamba msanii huyo alisubiri kwa muda wa miaka kumi kupata mtoto akiwa kwenye ndoa na sasa anasimulia aliyopitia binafsi kuhusu imani, uvumilivu na changamoto alizopitia kabla ya kupata mtoto wake wa kwanza.

“Msimu wetu wa kusubiri sio msimu wao wa kushindwa!” aliandika Wanjiru kwenye Instagram kwenye chapisho la kutangaza kitabu hicho.

Aliendelea kusema kwamba wakati mwingine tukiwa tunasubiri, Mungu anaandaa kitu kingine kikubwa kuliko hata tunavyofikiria. “Amini muda wake, shikilia imani na kamwe usipoteze matumaini,” aliandika.

Wanjiru na mumewe, Agundabweni Akweyu, walisubiri miaka kumi kabla ya kupata mtoto wao wa kiume, Mshindi, aliyezaliwa Aprili 6, 2022.

Kupitia kitabu hicho, Wanjiru anasimulia changamoto za kihisia zilizoambatana na safari yao, huku akisisitiza umuhimu wa imani, subira na matumaini wakati wa kukabili vipindi vigumu maishani.

Kitabu ‘The Wait’ pia kinalenga kuwatia moyo watu binafsi na wanandoa wanaopitia changamoto kama hizo, kikikumbusha wasomaji kuwa hali ngumu za maisha zinaweza kuwa chanzo cha nguvu na msukumo.

Kitabu hicho kinapatikana katika mfumo wa kidijitali kupitia jukwaa la Bwenieve Read, huku nakala zilizochapishwa zikipatikana kupitia Amazon na Nuria Kenya.

Share This Article