Hafla ya kutoa heshima kwa mwimbaji mkongwe wa Rwanda, Mariya Yohana, inapangwa jijini Kigali nchini Rwanda ili kutambua mchango wake wa miongo kadhaa katika muziki.
Shughuli hiyo ya Novemba 28, 2026, itatumiwa pia kutambua juhudi zake za kuhamasisha uzalendo, umoja na maridhiano nchini humo.
Kampuni ya muziki ya Country Records, itaandaa hafla hiyo katika hoteli ya Glimpse na inatarajiwa kuhudhuriwa na watu kati ya 300 na 350, wakiwemo wanamuziki wenzake na chipukizi.
Shughuli hiyo itajumuisha mjadala shirikishi utakaowapa wasanii vijana fursa ya kujifunza kutokana na safari ya Yohana katika muziki na uzoefu wake wa muda mrefu.
Yohana, aliyezaliwa mwaka 1943 kwa jina la Marie Jeanne Mukankuranga, alipata umaarufu kupitia nyimbo kama ‘Intsinzi’ na ‘Inkotanyi z’Amarere’.
Nyimbo zake ziliwatia moyo wapiganaji katika harakati za ukombozi wa Rwanda na baadaye kuhusishwa na matumaini na maridhiano ya kitaifa kufuatia mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994.
Mwaka 2007, alipokea Nishani ya Mapambano ya Ukombozi kutoka kwa Rais Paul Kagame na licha ya umri wake, Yohana anasema maendeleo ya Rwanda yanampa motisha wa kuendelea kutengeneza muziki.
Ushawishi wake bado unaonekana miongoni mwa wanamuziki vijana wa muziki wa jadi, huku wasanii mashuhuri wakisifu mchango wake wa kudumu katika kuhifadhi urithi wa muziki wa Rwanda.
Mwanzilishi wa Country Records, Nduwimana Jean Paul, alisema hafla hiyo inalenga kuheshimu urithi wa Yohana na kutambua namna anavyoendelea kuwa chanzo cha hamasa kwa vizazi mbalimbali vya wanamuziki.