Héritier Watanabe atangaza tamasha Nairobi

Atapanda jukwaani na bendi yake Oktoba 31, 2026, katika uwanja wa Carnivore jijini Nairobi.

Marion Bosire
1 Min Read

Gwiji wa muziki wa rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Héritier Watanabe, ametangaza rasmi ujio wa tamasha yake jijini Nairobi.

Nyota huyo ametumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kutangaza kwamba atatumbuiza nchini Kenya kwa mara ya kwanza katika tamasha inayotarajiwa kufanyika Jumamosi, Oktoba 31, 2026.

Katika tamasha hiyo kubwa mwanamuziki huyo atapanda jukwaani akiwa na bendi yake ya moja kwa moja, maarufu kama Team Wata, katika uwanja maarufu wa Carnivore jijini Nairobi.

Mashabiki wa muziki wa rhumba ya Congo na Soukous nchini Kenya wamekuwa wakisubiri kwa hamu tamasha yake kubwa tangu alipojizolea umaarufu akiwa mwanachama wa zamani wa bendi ya Wenge Musica Maison Mère.

Watanabe anatarajiwa kuwapa mashabiki burudani ya kukata na shoka, akichanganya midundo ya kusisimua na sauti yake nyororo.

Tiketi za tamasha hiyo tayari zimeanza kuuzwa kupitia tovuti ya Hustlesasa. Tiketi za kawaida zinauzwa shilingi elfu 5,huku za VIP zikiuzwa shilingi elfu 20. Mashabiki wanaotaka huduma za kifahari zaidi wanaweza kupata tiketi za VVIP kwa elfu 30.

Ingawa Watanabe hajawahi kushirikiana na wasanii wa Kenya awali, tangazo hilo tayari limezua msisimko mkubwa mitandaoni.

Mashabiki wanakisia kuhusu wasanii wa Kenya ambao huenda wakachaguliwa kutumbuiza kabla ya mwanamuziki huyo nyota wa Afrika kupanda jukwaani.

Share This Article