Mwanamuziki mkongwe wa Uganda, Jose Chameleone, ametangaza rasmi kurejesha tarehe yake ya Desemba 4, 2026 katika uwanja wa Lugogo Cricket Oval jijini Kampala.
Msanii huyo maarufu ataandaa tamasha yake inayosubiriwa kwa hamu ya “Chameleone Unlimited”.
Tangazo hilo linafuuatia miezi kadhaa ya mvutano katika tasnia ya muziki. Mnamo Mei, Chameleone alijitolea kuachia nafasi hiyo ambayo tayari ilikuwa imelipiwa kikamilifu kwa msanii mwenzake King Saha, akilenga kuendeleza umoja katika tasnia.
Hata hivyo, King Saha alikataa ombi hilo, akisema hakuwa na mpango wa kufanya onyesho siku hiyo. Chameleone, ambaye hivi karibuni amefanya ziara za muziki zilizofanikiwa nchini Kenya na Tanzania, sasa amerejesha rasmi nafasi hiyo.
Jose Chameleone analenga kuufanya kuwa usiku wa kihistoria, huku akiwaalika rasmi viongozi wa nchi za Afrika Mashariki, akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye.
Tamasha ya “Chameleone Unlimited” inatarajiwa kuanza saa 11:00 jioni, huku tiketi za kawaida zikianzia Shilingi elfu 20, pesa za Uganda, sawa na shilingi 650 za Kenya.
Inatarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki wa muziki kutoka Uganda na maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki katika uwanja huo maarufu wa burudani jijini Kampala.