Rais Ruto aagiza kupandishwa vyeo kwa walimu elfu 50

Serikali ilikuwa tayari imetangaza nafasi 34,016 za kupandishwa vyeo, lakini akaagiza idadi hiyo iongezwe hadi 50,000.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ameagiza walimu 50,000 wapandishwe vyeo, akipanua zoezi ambalo amelieleza kuwa kubwa zaidi la aina yake kuwahi kufanyika nchini Kenya ndani ya mwaka mmoja.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani katika Ukumbi wa Kasarani jijini Nairobi, Ruto alisema serikali ilikuwa tayari imetangaza nafasi 34,016 za kupandishwa vyeo, lakini akaagiza idadi hiyo iongezwe hadi 50,000.

Alisema ufadhili wa ziada utatolewa kusaidia zoezi hilo lililopanuliwa, hivyo kutimiza ahadi aliyowapa walimu mwaka uliopita.

Ruto alisema serikali pia imeongeza maradufu bajeti ya upandishaji vyeo kwa walimu kutoka Shilingi Bilioni 1 hadi Bilioni 2, huku mashauriano kati ya Tume ya Huduma za Walimu,TSC na vyama vya walimu kuhusu miongozo mipya ya maendeleo ya taaluma yakikamilika.

Rais alisema walimu 126,462 wamepandishwa vyeo tangu serikali yake iingie madarakani, ingawa alikiri kuwa walimu wengi wamekuwa katika daraja moja kwa miaka mingi.

Alisema kuboresha maendeleo ya taaluma ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha taaluma ya ualimu, pamoja na kuboresha huduma za afya, mishahara, makazi na pensheni.

Ruto pia alitangaza kuwa Shilingi Bilioni 4.9 zimetengwa kwa ajili ya kuajiri walimu 20,000 wa kandarasi ambao wamehudumu kwa miaka miwili katika ajira za kudumu na zenye pensheni kuanzia Januari 2027.

Aliwasifu walimu kama wajenzi wa taifa na kuwataka waendelee kukuza taaluma zao.

Share This Article