ODPP, OHCHR kushirikiana katika masuala ya haki za binadamu

Ushirikiano huo unahusu kukuza haki za kibinadamu, uwajibikaji na upatikanaji wa haki nchini Kenya.

Marion Bosire
2 Min Read

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP, imeimarisha ushirikiano wake na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu, OHCHR.

Ushirikiano huo unahusu kukuza haki za kibinadamu, uwajibikaji na upatikanaji wa haki nchini Kenya.

ODPP ilipokea ujumbe wa OHCHR ulioongozwa na Mwakilishi wa OHCHR nchini Kenya, Charles Kwemoi, ambapo mazungumzo yalijikita katika masuala ya uwajibikaji wa polisi, ukiukaji wa haki za kibinadamu, maandamano ya amani na maandalizi ya kipindi cha kabla ya uchaguzi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Renson Ingonga, Katibu wa Huduma za Mashtaka, Alloys Kemo, alikaribisha mwendelezo wa msaada wa OHCHR katika kujenga uwezo, kutoa usaidizi wa kiufundi na kuandaa sera.

Mkutano huo pia ulijadili Itifaki ya Mfano kwa Maafisa wa Utekelezaji wa Sheria kuhusu kukuza na kulinda haki za kibinadamu wakati wa maandamano ya amani.

Kemo alipendekeza mafunzo ya pamoja kwa waendesha mashtaka na maafisa wa utekelezaji sheria, warsha, kampeni za uhamasishaji wa umma na mipango ya kuimarisha uwajibikaji wa polisi pamoja na kushughulikia makosa ya uchaguzi.

Taasisi hizo mbili pia zilikagua ushirikiano unaoendelea katika kesi mbalimbali, ikiwemo kesi ya Baby Pendo, ambapo OHCHR imeunga mkono mchakato wa mashtaka unaozingatia mahitaji ya waathirika, pamoja na Uchunguzi wa Kifo cha Rex Masai.

Share This Article