Eddy Kenzo ammiminia Mesach Semakula sifa

Amesifu safari ya Semakula ya miongo kadhaa katika tasnia ya muziki.

Marion Bosire
2 Min Read
Eddy Kenzo

Msanii muziki nchini Uganda Eddy Kenzo amemmiminia sifa mwanamuziki mkongwe Mesach Semakula, akimtaja kuwa miongoni mwa watu muhimu katika historia ya muziki nchini Uganda.

Katika ujumbe mrefu aliochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Kenzo alisifu safari ya Semakula ya miongo kadhaa katika muziki.

Alielezea jinsi alivyotoka kuwa mwanamuziki kijana aliyekumbana na changamoto na kukataliwa jijini Kampala hadi kuwa mwimbaji, mtunzi wa nyimbo, mshauri na kiongozi wa bendi anayeheshimika.

Kenzo alisema mchango wa Semakula ni zaidi ya muziki wake, akibainisha nafasi yake katika maendeleo ya muziki wa bendi nchini Uganda kupitia Eagles Production na baadaye Golden Production.

Pia alimtaja kama mlezi wa wasanii vijana na mtu aliyesaidia kujenga mifumo iliyowezesha wasanii mbalimbali kuendeleza taaluma zao.

Kwa mujibu wa Kenzo, nyimbo za Semakula, zikiwemo Tukwegomba Bangi, Kulika Baby, First Aid, Sigwe Onsimila na Kankutendereze zimekuwa sehemu ya kumbukumbu ya muziki wa Uganda kwa kugusia mada kama vile mapenzi, familia, mahusiano na maisha ya kila siku.

Kenzo, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Kitaifa la Wanamuziki Uganda, UNMF, alisema Semakula anawakilisha uvumilivu, uthabiti na maisha marefu katika tasnia ya muziki.

Heshima hiyo imetolewa kabla ya tamasha ya Semakula ya kusherehekea miaka 50 katika tasnia ya muziki inayotarajiwa kufanyika Novemba 13, 2026, jijini Kampala.

Kenzo amesema tamasha hiyo itakuwa sherehe ya maisha ya Semakula, muziki wake, mchango wake katika kuwalea wasanii na nafasi yake katika kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa Uganda.

Share This Article