Rayvanny atania suala la Diamond na Upendo Nkone

Amechapisha video ya pamoja na Upendo Nkone na kuwataka wanaomwingilia wakome.

Marion Bosire
1 Min Read
Rayvanny

Msanii wa muziki nchini Tanzania Rayvanny anaonekana kuingiza utani katika suala zima la mvutano kuhusu dini kati ya mwimbaji wa nyimbo za injili Upendo Nkone na Diamond Platnumz.

Msanii huyo amechapisha video ya pamoja na Upendo Nkone na kuandika, “Mwacheni mama yangu… Na mshindwe mlegee, USHETANI WENU PELEKENI HUKOO,”.

Diamond ameongeza maoni yake chini ya chapisho hilo ambapo ameandika, “Mnafiki Fala wewe, Tena we ndio giza kabisa kaa mbali hapo,”.

Kumekuwa na mvutano kati ya wanaotumia mitandao ya kijamii nchini Tanzania, baada ya Upendo Nkone kuonekana kuwa kinyume na hatua ya mwimbaji mwenza Joel Lwaga kushirikiana na Diamond Platnumz katika wimbo, “Nikumbuke”.

Nkone alisisitiza kwamba watumishi wa Mungu hawapaswi kuchanganya mambo ya kiroho na ya dunia, akionya dhidi ya tamaa za mali, ikikumbukwa kwamba Diamond ambaye ni mwisilamu huimba nyimbo za dunia.

Wimbo ‘Nikumbuke’ ulizinduliwa Septemba 2026 na Lwaga akaamua kupanga hafla ya kusherehekea siku ya kuzaliwa Jumapili Septemba 27, 2026 akaipa jina la “Nikumbuke”.

Diamond Platnumz alihudhuria hafla hiyo katika eneo la Superdome Masaki jijini Dar es Salaam na alipohutubia waliokuwepo alimsifia Lwaga kwa kumtia moyo kumpenda Mungu.

Msanii huyo alisoma vifungo vya Biblia ambavyo ni Luka 5:31-32 na Matayo 9:10-13.

Share This Article