King Saha asusia kazi kisa ushauri wa madaktari

Msanii huyo aliugua na kushauriwa na madaktari wake apumzike na kupata nafuu kabla ya kurejelea kazi.

Marion Bosire
1 Min Read
King Saha

Msanii wa muziki nchini Uganda, King Saha, ametangaza kwamba hatajihusisha na kazi kama mwanamuziki kwa muda, kufuatia ushauri wa madaktari.

Haya yanajiri baada ya msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Ssemanda Manisul, kuugua na kushauriwa na madaktari wake apumzike na kupata nafuu kabla ya kurejelea kazi.

Katika taarifa kwa mashabiki wake, waendesha matukio na waandaaji wa maonyesho, mwimbaji huyo aliomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na hatua yake hasa kuhusiana na maonyesho yaliyokuwa yamepangwa kufanyika wiki hii.

“Ninaumwa kwa sasa, na madaktari wangu wamenishauri nipumzike hadi nitakapopata nguvu tena,” alisema Saha, akiongeza kuwa hatarudi jukwaani hadi atakapopona kikamilifu.

Msanii huyo pia aliwajibu wale walioathiriwa na kughairiwa kwa maonyesho yake, akisema marejesho ya fedha, pale yatakapohitajika, yatashughulikiwa baada ya kupona na kuhakikisha kuwa hali yake ya afya imetengemaa.

Saha aliwashukuru mashabiki na wafuasi wake kwa uvumilivu, uelewa na maombi yao wakati huu wa kupona.

“Afya ndiyo muhimu zaidi,” alisema katika ujumbe mwingine, akiwahakikishia mashabiki kwamba anachukua muda wa kupumzika kama alivyoelekezwa na madaktari.

Haya yanajiri wakati ambapo msanii huyo anatarajiwa kutumbuiza kwenye tamasha huko London pamoja na wasanii wenza Sheebah, T Paul na Winnie wa Mummy, Novemba 7, 2026.

Share This Article