Kamanda wa kitengo cha ulinzi wa watu mashuhuri amefariki

Opicho, alifariki akipokea matibabu katika hospitali moja Jijini Nairobi Jumatatu usiku.

Tom Mathinji
1 Min Read
Lazarus Opicho ameaga dunia.

Kamanda wa kitengo cha ulinzi wa majengo ya serikali na watu mashuhuri Msaidizi Mkuu wa Inspekta Jenerali wa Polisi Lazarus Opicho, ameaga dunia baada ya kuugua.

Opicho, alifariki akipokea matibabu katika hospitali moja Jijini Nairobi Jumatatu usiku.

Akimwomboleza Opicho, Jaji Mkuu Martha Koome alimtaja kuwa afisa wa polisi aliyejitolea mhanga katika utumishi wa umma, ulinzi wa majengo ya serikali na watu mashuhuri na wale waliotangamana na taasisi za serikali.

“Kwa niaba ya Idara ya Mahakama na mimi binafsi, natuma rambirambi kwa Ispekta Jenerali wa Polisi, uongozi wa Huduma ya Taifa ya Polisi, familia, na wafanyakazi wenza kutokana kifo hicho cha ghafla,” alisema Koome kwenye taarifa.

Koome alisema Opicho alikuwa kiongozi mwanzilishi wa kitengo cha Polisi wa Idara ya Mahakama mwaka 2021, kutoa ulinzi kwa maafisa wa idara hiyo, watumiaji wa mahakama na majengo ya mahakama kote nchini.

“Tutamkumbuka kwa kuongoza kitengo kipya, alisaidia kuweka msingi wa kitaasisi na kuchangia kwa maendeleo ya jinsi ya kushughulikia mahitaji ya kiusalama ya Idara ya Mahakama,” aliongeza Koome.

Jaji Mkuu huyo aliitakia familia ya Opicho nguvu wakati huu mgumu wa maombolezi ya mpendwa wao.

Share This Article