DCI yashirikiana na Uingereza kukabiliana na uhalifu wa uhamiaji

Amin alisema kubuniwa kwa kikosi cha kukabiliana na uhalifu wa uhamiaji, kumefanikisha kutambua, kuchunguza na kuharibu mtandao wa uhalifu unaohusiana na uhamiaji.

Tom Mathinji
2 Min Read

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imeshirikiana na Uingereza kusambaratisha mitandao ya wahalifu wanaofanikisha uhamiaji haramu.

Kwenye mkutano wa kukabiliana na uhalifu wa uhamiaji ulioandaliwa Moyale, kaunti ya Marsabit, Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin, alisema mji wa Moyale ni muhimu kwa kustawisha biashara, utangamano wa kijamii na fursa za kiuchumi, lakini akaonya dhidi ya mitandao ya wahalifu ambao hutumia usafiri kwenye maeneo ya mipaka kujinufaisha kwa njia haramu.

“Moyale ni kiingilio, mahali ambapo watu, familia, biashara na jamii hukutana, na kutafuta fursa halali za kiuchumi,” alisema Amin.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kamanda wa chuo cha Kitaifa cha Mafunzo kuhusu Upelelezi wa Jinai (NCIA) Ibrahim Jilo, Amin alisema kubuniwa kwa kikosi cha kukabiliana na uhalifu wa uhamiaji, kumefanikisha kutambua, kuchunguza na kuharibu mtandao wa uhalifu unaohusiana na uhamiaji.

Alitoa wito wa ushirikiano wa  pamoja miongoni mwa asasi zinazohudumu katika maeneo ya mpakani, katika kukabiliana na magenge ya wahalifu.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Balozi wa Uingereza nchini Kenya Dkt. Ed Barnett, aliyeongoza ujumbe wa Uingereza katika mkutano huo, alipongeza ushirikiano huo kati ya Kenya na Uingereza katika kukabiliana na uhalifu wa uhamiaji, huku juhudi zikiimarishwa kumaliza magenge ya wahalifu katika maeneo ya mpakani.

Alihakikisha kuwa Uingereza itaendelea kuunga mkono DCI na asasi zingine, katika kutambua, kuchunguza na kuangamiza uhalifu wa uhamiaji.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Maafisa wa ngazi za juu wa Polisi, asasi zinazoshirikiana na DCI na viongozi wa kijamii.

Share This Article