Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA nchini Tanzania, limewatoza faini ya Shilingi milioni tatu kila mmoja msanii Godfrey Tumaini maarufu kama Dudubaya na Mratibu Mkuu wa Tamasha ya Miaka 30 ya Bongo Flava.
Hatua hiyo inafuatia ukiukaji wa maadili unaodaiwa kutokea kwenye tamasha iliyofanyika Septemba 19, 2026, katika uwanja wa General Tyre, jijini Arusha.
Kwa mujibu wa BASATA, Dudubaya alikiuka mwongozo wa maadili katika kazi za sanaa na kutenda kosa linalokiuka heshima ya msikilizaji au mtazamaji, kinyume na Kanuni ya 20(a) ya Kanuni za BASATA, Tangazo la Serikali Na. 137 la Mei 22, 2026.
Baraza hilo limesema lilitathmini utetezi wa msanii huyo na kujiridhisha kuwa kosa lilitendeka kwa makusudi. Aidha, limedai kuwa amekuwa akikabiliwa na makosa yanayojirudia ya kukiuka taratibu za uendeshaji wa matamasha.
Mratibu Mkuu naye ameadhibiwa kwa kumtumia Dudubaya kutumbuiza katika tamasha hiyo, huku kosa la kimaadili likitokea wakati wa usimamizi wake.
Wote wametakiwa kulipa faini hizo ndani ya siku 14 na kusita kujihusisha na shughuli za sanaa hadi watakapotekeleza maamuzi hayo.
BASATA limewataka wasanii na wadau wote kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maadili katika utekelezaji wa shughuli za sanaa.
Dudubaya amekuwa akitumia kila fursa anayopata jukwaani kuzungumzia suala la ushoga akilikemea, hali ambayo inadaiwa kwenda kinyume na maadili.