Watu 17 wafariki kwenye ajali ya ndege DRC

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kuelekea Jiji Kuu Kinshasa, kutoka mji wa Kikwit siku ya Ijumaa ilipopata hitilafu za kiufundi na kujaribu kutua katika eneo la Kenge, mkoa wa Kwango.

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu 17 wafariki kwenye ajali ya ndege DRC.

Takriban watu 17 wamefariki wakiwemo maafisa wakuu wa jeshi, baada ya ndege ya kijeshi kuanguka Kusini Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kuelekea Jiji Kuu Kinshasa, kutoka mji wa Kikwit siku ya Ijumaa ilipopata hitilafu za kiufundi na kujaribu kutua katika eneo la Kenge, mkoa wa Kwango.

“Kutokana na ukosefu wa uwanja wa kutua kwa ndege katika eneo la Kenge, ndege hiyo ilianguka kwenye nyumba ya makazi,” alisema Naibu Gavana wa Kwango Remy Saki Bokinda.

Kulingana na Bokinda, ndege hiyo iliteketea baada ya kuanguka, akiashiria kuwa kinyume na idadi ya awali iliyotolewa ya watu 13, miili 16 ya watu wazima na moja ya mtoto ilipatikana na kufikisha idadi ya walioangamia kwenye ajali hiyo kuwa 17.

Taarifa ya jeshi la DRC, ilisema Majenerali wawili walikuwa wakisafiri kwenye ndege hiyo, ambao ni Luteni Jenerali Joseph Mutombo na Luteni  Lucien-Rene Likulia.

Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi, ameagiza uchunguzi wa kina kubainisha chanzo cha ajali hiyo.

Tshisekedi alituma rambirambi kwa familia za walioangamia kwenye ajali hiyo pamoja na kwa maafisa wote wa usalama.

Share This Article