Rais Xi wa China awasili Marekani kwa ziara ya kiserikali

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Xi nchini Marekani tangu mwaka 2023 alipohudhuria mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki jijini San Francisco.

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais Xi na mkewe Peng Liyuan / Picha kwa hisani ya CGTN

Rais China Xi Jinping amewasili nchini Marekani kwa ziara ya kiserikali nchini humo.

Rais Xi na mkewe Peng Liyuan waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Andrews jana Jumatano mchana.

Punde baada ya kuwasili, walilakiwa na mwenyeji wao, Rais Donald Trump wa Marekani pamoja na mkewe Melania Trump uwanjani hapo.

Hafla ya mapokezi ilijumuisha ufyatuaji wa mizinga ya heshima na upigaji wa nyimbo za taifa za nchi zote mbili.

Kwenye hotuba yake ya maandishi, Rais Xi amesema China na Marekani zinapaswa kuwa washirika, badala ya wapinzani.

Ameongeza kuwa dira ya China ya kutimiza ustawi mpya wa taifa na ajenda ya Marekani ya kufanya nchi hiyo kuwa na nguvu zaidi (MAGA) vinaweza kwenda sambamba na kukamilishana, jambo ambalo litanufaisha dunia nzima.

Hafla ya kumkaribisha Rais Xi imepangwa kufanyika leo Alhamisi katika Ikulu ya Marekani, ikifuatiwa na mkutano kati ya viongozi hao wawili na kisha dhifa ya kitaifa.

Masuala ya kiuchumi na biashara yanatarajiwa kutawala ajenda kuu ya mkutano wao.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Xi nchini Marekani tangu mwaka 2023 alipohudhuria mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki jijini San Francisco.

Taarifa hii imechangiwa na CGTN

Share This Article