Kenya imechagua “One Woman, One Bra” kuwa filamu yake rasmi ya kuwasilishwa katika kitengo cha Filamu Bora ya Kimataifa kwenye Tuzo za 99 za Akademia, almaarufu Oscars.
Tangazo hilo limetolewa leo Septemba 23, 2026, na Kamati ya Kenya ya Uteuzi wa Oscars, baada ya kupitia filamu tatu zilizowasilishwa kwa ajili ya kuzingatiwa.
One Woman, One Bra ambayo imeundwa kwa jamii ya Maasai, ilichaguliwa kutokana na usimulizi wake halisi, uigizaji pamoja na uwasilishaji wa mandhari na urithi wa kitamaduni wa Kenya.
Kamati pia iliangazia ubunifu wa filamu hiyo, mtiririko wa simulizi, mavazi na usanifu wa sauti, unaojumuisha sauti zinazohusishwa na maisha ya jamii ya Maasai, wakiwemo ng’ombe na kengele za ng’ombe.
Mchakato wa uteuzi ulihitaji filamu itimize kanuni za kiufundi za Akademia, likiwemo sharti la kuwa na zaidi ya asilimia 50 ya maudhui katika lugha ya wenyeji.
Mwenyekiti wa Kamati, Eddah Kiruhi, alisema filamu hiyo inawakilisha usimulizi halisi kutoka ndani ya jamii ya Maasai na kuonyesha ubunifu pamoja na simulizi zinazochipuka nchini Kenya.
Kamati ilisema filamu hiyo ina lugha ya kisanaa iliyokita mizizi katika uzoefu wa Kenya huku ikiwa na uwezo wa kuwafikia watazamaji wa kimataifa.
Uteuzi huo ni hatua nyingine kwa Kenya katika kutafuta kutambulika katika jukwaa la kimataifa la filamu.
Tume ya Filamu Kenya, KFC hutoa usaidizi wa sekretarieti kwa kamati hiyo huru ya uteuzi, inayofanya kazi kwa mujibu wa kanuni za Academy.