Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), imetwaa shilingi 708,664 kutoka kwa afisa wa zamani wa serikali ya kaunti ya Homa Bay kwa madai ya kupokea mshahara maradufu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Hatua hiyo imetokana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Septemba 18, 2026.
Fedha hizo zilitwaliwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi kuhusu malipo maradufu ya mishahara kwa wafanyakazi wa sasa na wale wa zamani wa serikali ya kaunti hiyo.
Uchunguzi huo ulibainisha kuwa Evelyn Ogweno, alipokea mshahara maradufu kati ya Februari 2015 na Mei 2018, ambapo alipokea shilingi 708,664 zaidi ya mshahara wake.
Upatikanaji wa fedha hizo ni sehemu ya kesi zilizowasilishwa na EACC, kufuatia uchunguzi wa madai ya kupotea kwa shilingi 42,249,988 kupitia mfumo wa malipo katika serikali ya kaunti ya Homa Bay.