Afisa Mkuu wa uangalizi anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya kukabiliana na ufisadi ya Milimani, kwa madai ya kupokea hongo ya shilingi 150,000, ili avuruge matokeo ya kesi ya uhalifu katika mahakama ya Kangema.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Tume ya Maadili na Kupamabana na ufisadi (EACC), ilisema Julius Irungu Njogu atafunguliwa mashtaka ya kupanga kutekeleza uhalifu wa ufisadi pamoja na kupokea hongo.
Mashtaka hayo yanafuatia uchunguzi uliotekelezwa kuhusiana na madai kwamba yeye pamoja na Hakimu mmoja Mkuu walipokea pesa ili kuvuruga matokeo ya kesi moja ya uhalifu.
Kulingana na tume hiyo, Njogu awali alikamatwa pamoja na Hakimu Mkuu Mwandamizi Martin Kinyua Mutegi, wakati wa uchunguzi huo.
Aidha, EACC imesema wawili hao waliachiliwa na bondi ya polisi, huku uchunguzi kuhusu swala hilo ukiendelea.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Njogu alikamatwa tena, ili afikishwe kwenye mahakama ya kukabiliana na ufisadi ya Milimani.
Wakati huohuo, EACC ilidokeza kuwa Hakimu huyo Mkuu Mwandamizi pia alitarajiwa kufikishwa mahakamani leo Jumanne, lakini alienda mafichoni. Hata hivyo baada ya Tume hiyo kumsaka, hakimu huyo alienda hospitalini na kulazwa.
“Tume hii itachukua hatua zote za kisheria kuhakikisha hakimu huyo anafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kupokea hongo ili kuvuruga matokeo ya kesi ya uhalifu,” ilisema EACC.