Museveni atimiza ahadi aliyowapa wanaoandaa matamasha

Badala ya kugawanywa kwa usawa miongoni mwa watu binafsi, fedha hizo zitatolewa kama mikopo kwa wabunifu ikiwa na kiwango cha chini cha riba.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametimiza ahadi yake ya kifedha kwa sekta ya burudani kwa kutoa Shilingi bilioni 10 kwa waandaaji wa muziki na matamasha ya ndani.

Fedha hizo zimetolewa kupitia Kituo cha Kusaidia Huduma Ndogo za Kifedha, MSC kama ruzuku yenye lengo la kukuza tasnia hiyo.

Pesa hizo zimegawanywa kati ya vyama vikuu vitatu vya ushirika wa akiba na mikopo yaani SACCOs, ambavyo ni Uganda Music Promoters SACCO, inayoongozwa na mwaandaaji mashuhuri Abbey Musinguzi au Abitex, United Music Promoters SACCO na National Events and Bivulu Promoters Multipurpose Cooperative.

Tangazo rasmi lilitolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika katika Hoteli ya Pope Paul Memorial huko Ndeeba, Kampala.

Badala ya kugawanywa kwa usawa miongoni mwa watu binafsi, fedha hizo zitatolewa kama mikopo kwa kiwango cha chini cha riba cha asilimia 8 kwa mwaka.

Kamati maalum ya mikopo itakagua maombi kulingana na uwezo wa kibiashara.Ili kuzuia migogoro ya usimamizi iliyotokea hapo awali, MSC imetoa mafunzo ya uongozi na elimu ya fedha kwa viongozi wakuu wa SACCO hizo.

Maafisa wa serikali walisisitiza kuwa fedha hizo zitafuatiliwa kwa makini ili kuhakikisha uwajibikaji wa wazi, uendelevu wa biashara, na uzalishaji wa nafasi za kazi katika sekta nzima ya burudani.

Museveni alitoa ahadi hiyo mwaka jana katika mkutano wa kimkakati na waandaaji muziki na wadau wa sekta ya burudani katika uwanja wa Kololo jijini Kampala.

Share This Article