Mwenda Nyaga nambari 2 mashindano ya kuzungumza Afrika

Aliwapiku washiriki wengine 11 kwenye fainali ya mwaka huu ya mashindano hayo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa asili ya kenya Mwenda Nyaga amemaliza katika nafasi ya pili kwenye fainali za mashindano ya kuigiza mwenyewe jukwaani almaarufu ‘Africa Monologue Challenge’.

Hafla hiyo ambayo ilikuwa msimu wa tatu wa mashindano hayo, iliandaliwa kwenye ukumbi wa maonyesho ya sanaa wa Accra nchini Ghana Ijumaa, Septemba 18, 2026 ambapo raia wa Ghana William Lampety aliibuka mshindi.

Tukio hilo lililowakutanisha washiriki 12 kutoka mataifa 12 na nje ya Afrika, lilihusisha washindani kutoka Ghana, Nigeria, Afrika Kusini na Marekani.

Wakishindana chini ya kaulimbiu “Uchumi wa Ubunifu wa Afrika kama Chombo cha Maendeleo na Umoja,” washiriki waliwasilisha maonyesho yenye nguvu yaliyolenga kuonyesha vipaji vya bara Afrika katika usimulizi wa hadithi na kukuza ushirikiano wa Waafrika.

Mashindano ya Africa Monologue Challenge yalizinduliwa rasmi Aprili 5, 2022, mjini Accra, Ghana. Yalianzishwa kwa ushirikiano wa kampuni ya uigizaji ya M.K. Casting, baraza la watayarishaji maudhui Afrika na Mamlaka ya kitaifa ya filamu nchini Ghana.

Lengo lake ni kuonyesha vipaji mbalimbali vya waigizaji wa Afrika, kuwalinganisha na viwango vya uigizaji vya Hollywood na kuwasaidia kupata fursa muhimu katika soko la kimataifa.

Nafasi ya pili ya Nyaga inaendeleza historia nzuri ya Kenya katika mashindano hayo.

Katika msimu wa kwanza Kenya iliwakilishwa na Nyokabi Macharia na nyota wa Supa Modo, Stycie Waweru, huku Esther Wanjiru akishiriki msimu wa pili pamoja na mkurugenzi maarufu wa kuainisha waigizaji nchini Kenya, Gerald Langiri, aliyekuwa jaji wa Afrika nzima.

Share This Article