Ruto kupendekeza ajenda ya uwekezaji ya Kenya katika UNGA

Kulingana na Ikulu, Rais Ruto atatafuta ushirikiano katika sekta mbali mbali kwenye mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Marion Bosire
2 Min Read
William Ruto - Rais wa Kenya.

Rais William Ruto ameondoka nchini kuelekea New York, Marekani, kuhudhuria Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA.

Akiwa katika mkutano huo, Rais atapendekeza ajenda ya uwekezaji ya Kenya, kuvutia mitaji na kuimarisha nafasi ya Afrika katika uchumi wa kidijitali na teknolojia ya akili unde duniani.

Kulingana na Ikulu, Rais Ruto atatafuta ushirikiano katika sekta za nishati, miundombinu, uzalishaji, afya, kilimo na teknolojia, kwa lengo la kuunda ajira, kuongeza uzalishaji na kufungua masoko mapya.

Atakuwa mwenyekiti mwenza wa mikutano ya kibiashara iliyoandaliwa na Shirika la Fedha la Afrika, AFC na Mpango wa Dunia Kuhusu Biashara Afrika, GABI pamoja na mfanyabiashara wa asili ya Nigeria, Aliko Dangote.

Ajenda kuu itakuwa mradi unaopendekezwa wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Shilingi Trilioni 2.2 sawa na Dola Bilioni 17 huko Lamu, chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku na kinachotarajiwa kuunda nafasi za ajira zaidi ya elfu 60.

Ujenzi umepangwa kuanza Septemba 30, 2026.

Rais Ruto pia ataongoza kwa pamoja na Rais wa Finland Alexander Stubb, mpango wa Mamlaka za Wastani za Akili Unde , huku akiendeleza mpango wa Akili Unde wa gharama ya Shilingi Bilioni 10 unaoungwa mkono na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Atasisitiza pia mkakati wa “Afrika kufadhili Afrika”, akiangazia zaidi akiba ya ndani ya bara hili ya dola trilioni 4, bila kusahau Hazina ya Kitaiga ya Kufadhili Miundombinu, NIF, uwekezaji wa ughaibuni na ushirikiano katika miradi ya teknolojia atakapokutana na viongozi mbali mbali wa ulimwengu, Taasisi na Biashara.

Share This Article