Wawili wafariki, kadhaa wajeruhiwa ajali ya lori la mafuta Eldoret

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu walifika eneo la mkasa kuwaokoa manusura wakishirikiana na wale wa kutoka kitengo cha zima moto.

Dismas Otuke
1 Min Read

Watu wawili wameripotiwa kuaga dunia huku wengine 10 wakipokea matibabu katika hospitali mbalimbali  kufuatia mkasa wa moto wa lori la mafuta uliotokea Alhamisi usiku.

Mkasa huo ulitokea karibu na shule ya sekondari ya Paul Boit kwenye barabara ya Eldoret-Turbo.

Lori hilo lilibingiria kabla ya kushika moto huku majeruhi wakichomeka kwa kiwango kikubwa.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa eneo la Bonde la Ufa Samuel Ndanyi, miili ya watu wawili ilitolewa katika eneo la ajali.

Yamkini watu hao walikuwa wamekimbia eneo la mkasa kuchota mafuta baada ya lori hilo kuanguka na punde moto ukazuka.

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu walifika eneo la mkasa kuwaokoa manusura wakishirikiana na wale wa kutoka kitengo cha zima moto.

Moto huo ulizimwa kufikia Ijumaa saa kumi alfajiri na idadi kamili ya majeruhi haijabainika.

 

Share This Article