Watu wapatao watano waliripotiwa kufariki katika ajali iliyotokea katika eneo la Athi River, kaunti ya Machakos kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa jana Jumatano usiku.
Kulingana na ripoti ya polisi, ajali hiyo ilitokea majira ya saa moja na dakika 40 usiku, ikihusisha matatu ya chama cha Kinatwa na lori la Isuzu.
Shuhuda alisema matatu hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Mombasa kuelekea Nairobi wakati dereva alipojaribu kuyapita magari mengine kiholela na ikakutana uso kwa uso na lori.
Walioaga dunia papo hapo ni pamoja na dereva wa matatu na abiria wanne.
Polisi wamesema abiria wengine saba walipata majeraha na kukimbizwa katika hospitali ya Machakos Level Five Hospital wanakopokea matibabu.