Olu Jacobs afariki

Mke wake, ambaye pia ni mwigizaji mkongwe Joke Silva, ndiye alitangaza kifo chake.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji mkongwe wa filamu za Nigeria Olu Jacobs, ambaye kazi yake ilidumu kwa miongo kadhaa katika tamthilia, televisheni na filamu, amefariki akiwa na umri wa miaka 84.

Mke wake, ambaye pia ni mwigizaji mkongwe Joke Silva, ndiye alitangaza kifo chake na kuomba faragha familia inapoomboleza.

Silva alitangaza hayo kupitia taarifa iliyomtaja mwigizaji huyo mashuhuri kama “The Lion of Lufodo” yaani ‘Simba wa Lufodo’ akisema aliishi vyema na alipambana hadi mwisho.

Baadhi ya filamu zake maarufu ni pamoja na My Kingdom, Covert Operation na One Fine Day.

Jacobs alitambuliwa kama mmoja wa waasisi na watu waliokuwa nguzo za tasnia ya filamu nchini Nigeria Nollywood na aliheshimiwa na kupendwa kote nchini humo.

“Tunawaomba wanablogu na washawishi wote wa mitandao ya kijamii kuheshimu faragha ya familia yetu wakati huu,” Silva alisema katika taarifa hiyo.

Jacobs alizaliwa Julai 11, 1942, akasomea uigizaji katika taasisi ya Royal Academy of Dramatic Art mjini London. Baadaye alianza kazi ambapo alishiriki katika vipindi vya televisheni vya Uingereza pamoja na filamu za kimataifa.

Hatimaye, akawa mmoja wa watu muhimu katika maendeleo ya tasnia ya filamu ya Nigeria, akishiriki katika uzalishaji wa kazi nyingi za sanaa nchini Nigeria na kujijengea sifa kutokana na uwezo wake wa kuigiza na kubadilika katika majukumu mbalimbali.

Kazi yake ilidumu kwa zaidi ya miaka 50, ambapo alipokea tuzo na heshima mbalimbali, ikiwemo African Movie Academy Award ya Muigizaji Bora katika Jukumu Kuu na tuzo za kutambua mchango wake wa maisha katika sanaa.

Mwaka 2011, Jacobs alitunukiwa heshima ya kitaifa ya Member of the Order of the Federal Republic (MFR) kwa mchango wake katika tasnia ya filamu ya Nigeria.

Jacobs na Silva kwa pamoja walianzisha Lufodo Group na Lufodo Academy of Performing Arts, taasisi zilizochangia katika filamu na televisheni, pamoja na kukuza na kutoa mafunzo kwa wasanii wa sanaa za maonyesho nchini Nigeria.

Katika miaka ya hivi karibuni, Jacobs alikuwa amejitenga kwa kiasi kikubwa na shughuli za hadharani kutokana na changamoto za kiafya.

Share This Article