Kenya imeteuliwa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Riadha Duniani yatakayoandaliwa mwaka 2029.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa mashindano hayo kuandaliwa barani Afrika.
Kenya iliteuliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo baada ya kushinda nchi za Uingereza, Italia na Ujerumani ambazo pia zilikuwa zimetuma maombi.
Hata hivyo, Ujerumani ina kila sababu ya kutabasamu baada ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo mwaka 2031, miaka miwili tu baada ya mashindano hayo kuandaliwa nchini.
Nchini Kenya, Mashindano ya Riadha Duniani 2029 yataandaliwa katika uwanja uliokarabatiwa wa Kasarani.
Uteuzi wa Kenya umepokelewa vema na Wakenya wengi wakiongozwa na Rais William Ruto.
“Mashindano ya Riadha Duniani yanakuja nyumbani! Nchi yetu imeshinda haki ya kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Riadha Duniani 2029, na kuifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza kuandaa mashindano hayo ya dunia barani Afrika,” alisema Rais Ruto kwenye taarifa.
“Huu ni wakati wa Kenya, wakati wa Afrika na ushindi kwa vizazi vya wanariadha walioifanya nchi yetu kutambulika kwa mbio.”
Rais Ruto amepongeza timu iliyowasilisha ombi la Kenya, Wizara ya Michezo, wanariadha na yeyote aliyechangia Kenya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.