Kenya imepata wadhifa mwingine wa ngazi za juu kimataifa, kufuatia kuteuliwa kwa balozi Martin Kimani kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala ya Afrika katika idara za siasa na operesheni za kuleta amani (DPPA-DPO).
Uteuzi huo ulitangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, huku Kimani akichukua wadhifa ulioshikiliwa na Ama Akyaa Pobee wa Ghana.
Afisi hiyo ya DPPA, imejukumiwa kuimarisha juhudi za Umoja wa Mataifa katika utatuzi wa migogoro na kuleta amani kote duniani.
Kimani ana uzoefu wa kazi wa miaka 25 katika uhusiano wa kimataifa, amani na usalama na diplomasia ya kimataifa katika mashirika ya kikanda, serikali, mashirika yasiyo ya serikali na sekta ya kibinafsi.
Awali, Kimani alikuwa mwakilishi wa kudumu katika afisi ya Umoja wa Mataifa Jijini New York Marekani kati ya mwaka 2020- 2024.
Wakati wa kipindi cha Kenya kuwa mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 2021 na 2022, Kimani alihudumu wadhifa wa Rais wa Baraza hilo mwezi Oktoba mwaka 2021.
Mwaka 2023, Kimani alihudumu wadhifa wa Rais wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Hazina ya Idadi ya watu ya Umoja wa Mataifa na afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu huduma za miradi.
Aidha, alihudumu kama mkurugenzi wa kituo cha kitaifa cha kukabiliana na ugaidi nchini Kenya, na mjumbe maalum wa Rais wa kukabiliana na itikadi kali kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.