Maafisa wa Polisi wamemkamata mshukiwa mwingine anayedaiwa kuhusika kwenye ghasia zilizoghubika mkutano wa kisiasa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kaunti ya Embu juma lililopita.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), mshukiwa huyo alikamatwa Jumatatu katika eneo la Kithimu, Embu mjini kwenye operesheni iliyotekelezwa maafisa kutoka Makao Makuu ya DCI, Nairobi.
Kukamatwa kwake kunajiri huku maafisa wa upelelezi wakiimarisha juhudi za kuwatambua na kuwakamata washukiwa wanaoaminika kushiriki kwenye ghasia hizo.
“Wale waliohusika kwenye ghasia hizo, bila kuzingatia miegemeo yao, watatambuliwa, watakamatwa na kufunguliwa mashtaka,” ilisema DCI kupitia kwa taarifa.
Ghasia zilizuka kwenye mkutano huo uliokuwa ukiongozwa na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Gavana wa Embu aliyepia mwenyekiti cha chama cha UDA Cecily Mbarire.