Wanasiasa watakiwa kueneza sera, siyo migawanyiko

Wanasiasa wametakiwa kunadi sera na maono yao kwa Wakenya badala ya kujiingiza katika siasa za kueneza chuki na migawanyiko.

Martin Mwanje
3 Min Read
Mwenyekiti wa NCIC Dkt. Kepha Omae akihutubia Kongamano la Amani jijini Nairobi

Wanasiasa humu nchini wametakiwa kutilia mkazo masuala ya manufaa kwa taifa kwenye mikutano yao badala ya kujiingiza kwenye siasa za migawanyiko na kueneza chuki. 

Mwenyekiti wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, Dkt. Kepha Omae aidha amesisitiza umhimu wa kudumisha umoja nchini takriban mwaka mmoja kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu ujao.

“Kosoa sera, siyo jamii. Pinga mawazo, siyo utambulisho. Hebu kila msimu wa kampeni uwe mashindano ya maono, siyo mashindano ya migawanyiko,” alishauri Dkt. Wamae.

“Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 unatupa fursa ya kuonyesha kwamba amani ni kiwezeshi muhimu cha demokrasia. Lazima tuchague uzuaiaji badala ya uitikiaji na umoja badala ya umaarufu wa kisiasa.”

Dkt. Omae aliyasema hayo wakati akihutubia kongamano la siku mbili la amani lililong’oa nanga leo Jumatatu jijini Nairobi.

Kongamano hilo linawaleta pamoja wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na maafisa kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Idara ya Mahakama, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa na maafisa wa usalama.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Gilbert Masengeli alito wito wa kila Mkenya kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha usalama unadumishwa nchini wakati wote. 

“Usalama unaanza na wewe. Uchaguzi wa amani hauwezi kulindwa na asasi za usalama pekee; unahitaji wananchi kufanya kazi na wadau wa usalama na kuwajibikia taarifa wanazopokea na kueneza,” alisema Masengeli wakati akilalamikia visa vya uhuni vinavyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox alitoa wito kwa wadau wote daima kuheshimu sheria kwa manufaa ya nchi.

“Pamoja, tunaweza tukabadilisha mwelekeo kutoka njia hatari na uharibifu na badala yake kuchagua utawala wa sheria, ushirikiano, uwajibikaji na amani. Uchaguzi utakuja na kwenda, lakini Kenya itasalia,” alisema Cox.

Kadhalika wanasiasa walitakiwa kuchunga ndimi zao la sivyo wanaweza kuwa tishio kwa utangamano wa kitaifa.

“Lazima tuwakumbushe wanasiasa wetu kwamba hakuna mwanasiasa ambaye ni mkubwa kuliko Kenya, na hakuna chama cha kisiasa ambacho ni kikubwa kuliko Kenya. Kenya daima inakuja kwanza,” alisema Askofu Geoffrey Njuguna.

Lengo la kongamano hilo lenye kaulimbiu “Amani Kenya”, ni kujadiliana mbinu bora za kudumisha amani kwa kuhakikisha hata punje ya vurugu haishuhudiwi nchini wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Share This Article