Mwanamuziki wa Bongo Fleva, kutoka Tanzania, Marioo, ameshinda tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Eneo la Afrika Mashariki, katika tuzo za AFRIMMA mwaka 2026, zilizofanyika jana Septemba 12, 2026, huko Dallas, Texas, Marekani.
Marioo alitwaa tuzo hiyo baada ya kushindana na baadhi ya wasanii wakubwa kutoka Afrika Mashariki, akiwemo Diamond Platnumz, Juma Jux, Mbosso na Barnaba kutoka Tanzania, Bien wa Kenya, Eddy Kenzo na Joshua Baraka wa Uganda, Lij Michael wa Ethiopia pamoja na Single Dee wa Sudan Kusini.
Ushindi huo umeongeza mafanikio katika muziki kwa Marioo, ambaye pia alikuwa miongoni mwa wasanii wa Tanzania waliotarajiwa kutumbuiza katika tamasha ya muziki ya AFRIMMA, iliyofanyika Annette Strauss Square jijini Dallas.
Tuzo za AFRIMMA hutambua wasanii, nyimbo, maonyesho na wadau wengine wanaochangia ukuaji, maendeleo na ushawishi wa muziki wa Afrika duniani.
Ushindi wa Marioo unaendelea kuonyesha nafasi inayozidi kuimarika ya muziki wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa.