Serikali imeapa kuhakikisha inalinda fursa za kiuchumi za raia wake hasa katika sekta ya biashara ndogo ndogo.
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed anasema nchi hii iko tayari kwa wawekezaji wa kigeni kuja na kuendesha biashara zao alimradi wanafanya hivyo kwa kutii sheria zilizowekwa.
“Kenya italinda fursa za kiuchumi za raia wake, hasa ndani ya sekta ya biashara ndogo ndogo, wakati ikisalia tayari kwa uwekezaji, biashara na ajira za kigeni ambazo ni halali. Dhamira hizi ni za kukamilishana na zitafuatiliwa kwa mujibu wa katiba, sheria na majukumu ya kimataifa ya Kenya ,” alisema Hussein kwenye taarifa.
“Dhamira kya Kenya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, utangamano wa kikanda na umoja wa bara la Afrika inasalia thabiti.”
Serikali ya Kenya ikiahidi kuwa itaendelea kuwezesha usafiri wa watu, kazi, huduma na mtaji kwa mujibu wa mipangokazi husika ya kisheria na udhibiti, wakati ikiendeleza utangamano wa kikanda kupitia makubaliano ya eneo la biashara huru miongoni mwa mataifa ya Afrika, AfCFTA na sheria zingine za ushirikiano wa Afrika.
Aidha, serikali imeahidi kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa kigeni kusajili biashara zao na kupata vibali vinavyohitajika katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ili kuhakikisha wanatii sheria zilizowekwa za Kenya.
Taarifa hiyo inakuja wakati kumekuwa na mjadala mkali kuhusiana na kauli zinazodaiwa kutolewa na Rais William Ruto zikiashiria kuwa serikali itafanya msako dhidi ya raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo humu nchini.
Ripoti hizo zikiashiria kuwa serikali itawafurusha raia kama hao ili kuwaachia Wakenya biashara ndogondogo wakati ikiwapisha wawekezaji wenye mtaji mkubwa.
Ni madai ambayo serikali imekanusha vikali ikisema kila raia wa kigeni yuko huru kufanya biashara nchini alimradi awe na nyaraka na leseni zinazohitajika za kufanya biashara hiyo nchini.