Watengenezaji filamu wa Kenya wahimizwa kuwasilisha kazi zao kwa Oscars

Tarehe ya mwisho ya mawasilisho ni Septemba 11, 2026

Marion Bosire
2 Min Read

Watengenezaji filamu wa Kenya wamehimizwa kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya tuzo za akademia almaarufu Oscars kabla ya makataa kukamilika.

Wito huu umetolewa na Tume ya Filamu Nchini, KFC, zikiwa zimesalia siku tatu pekee kabla ya tarehe ya mwisho ya kuwasilisha ambayo ni Septemba 11, 2026.

Tume ya Filamu ya Kenya inawataka watengenezaji filamu wanaostahiki kutumia fursa hii kuonyesha hadithi na vipaji vya Kenya katika jukwaa la kimataifa.

Watengenezaji filamu ambao bado hawajawasilisha kazi zao wanahimizwa kukamilisha mawasilisho yao, kupitia masharti ya ushiriki na kuhakikisha kuwa nyaraka na vifaa vyote vinawasilishwa kabla ya tarehe ya mwisho.

Tume inawahimiza watengenezaji filamu kutokosa fursa ya kazi zao kuzingatiwa kwa mojawapo ya tuzo za filamu zinazoheshimika zaidi duniani.

Zikiwa zimebakia siku tatu pekee, watengenezaji filamu wanahimizwa kuchukua hatua sasa na kuwasilisha filamu zao kwa wakati kupitia kaulimbiu, ‘Wasilisha filamu yako. Iwakilishe Kenya. Uutie moyo ulimwengu’.

Huku watengenezaji filamu wa Kenya wakiharakisha kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya kuzingatiwa katika Tuzo za Oscars, safari ya Kenya katika Oscars inaonyesha azma inayoongezeka na changamoto zinazoikabili sekta ya filamu nchini.

Kenya imewahi kuwasilisha filamu tisa kwa ajili ya kuzingatiwa katika kipengele cha Filamu Bora ya Kimataifa, mawasilisho ya kwanza yakiwa ya mwaka 2012.

Filamu hizo ni Nairobi Half Life, Kati Kati, Supa Modo, Subira, The Letter, Mission to Rescue, TeraStorm, Mvera na Nawi.

Licha ya kuongezeka kwa idadi ya filamu zinazowasilishwa, hakuna filamu ya Kenya ambayo hadi sasa imepata uteuzi wa mwisho katika kipengele cha Filamu Bora ya Kimataifa katika Oscars.

Share This Article