Mudavadi ahimiza Afrika kutumia zaidi mtaji wake kusukuma maendeleo

Alizungumza jijini Nairobi alipomwakilisha Rais William Ruto katika uzinduzi wa wiki ya kongamano la kwanza la mtaji barani Afrika.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi, amezitaka nchi za Afrika kutumia zaidi mitaji yao ya ndani kufadhili maendeleo, kuunda ajira na kuimarisha uhuru wa kiuchumi wa bara hili.

Alikuwa akizungumza jijini Nairobi alipokuwa akimwakilisha Rais William Ruto katika uzinduzi wa wiki ya kongamano la kwanza la mtaji barani yaani, Africa Capital Week 2026.

Katika mkutano huo, Mudavadi alisema Afrika ina rasilimali kubwa za kifedha zinazoweza kuelekezwa katika biashara, miundombinu na kuunda fursa kwa idadi yake inayoongezeka ya watu.

Kulingana naye, wawekezaji wa taasisi barani Afrika wanadhibiti mali za thamani ya zaidi ya dola trilioni 1.1 za Marekani, akitaja kiwango hicho kuwa fursa kubwa kwa bara hili kufadhili maendeleo yake lenyewe.

Mudavadi alisema uhuru wa kiuchumi haupaswi kumaanisha kuitenga Afrika na masoko ya kimataifa, bali kulishirikisha bara hili katika masoko hayo likiwa katika nafasi imara, likiungwa mkono na masoko ya mitaji yaliyoimarika, taasisi thabiti na miradi iliyo tayari kwa uwekezaji.

Alisema Kenya iko tayari kushirikisha uzoefu wake katika mageuzi ya soko la mitaji na kushirikiana na wadau kuimarisha uwezo wa Afrika kukusanya na kutumia rasilimali zake.

Mudavadi aliwataka wadau kuachana na mijadala na ahadi pekee na kuelekea katika utekelezaji wa miamala halisi, uwekezaji na kutumia mitaji kuleta maendeleo barani Afrika.

Vikao vya kongamano hilo lenye kaulimbiu, “Kuimarisha Masoko ya Mitaji ili Kuendeleza Uhuru wa Kiuchumi wa Afrika” vitafanyika Septemba 7 hadi 8, 2026 katika Hoteli ya The Argyle Grand jijini Nairobi.

Washiriki watapata fursa ya kuzuru masoko na maeneo ya miradi kuanzia Septemba 9 hadi 11, 2026.

Share This Article