Msanii wa muziki wa asili ya Burundi, Kidum, ametangaza kwamba ametoa gari lake lenye uwezo wa kubeba abiria 11, kusaidia raia wa Burundi wanaotaka kurejea nyumbani kufuatia madai ya kushambuliwa na kunyanyaswa nchini Kenya.
Kidum, ambaye ameishi Kenya tangu 1995 na kuichukulia nchi hii kuwa nyumbani, alitoa wito wa utulivu na suluhisho la kidiplomasia.
Alisema amepokea picha za kusikitisha kutoka Nairobi zinazoonyesha madai ya unyanyasaji dhidi ya raia wa Burundi na Rwanda yanayoaminika kuchochewa na maelekezo ya Rais William Ruto kuhusu taratibu za wageni kuishi, kufanya kazi na kufanya biashara nchini.
Msanii huyo anataka Waburundi warejee nyumbani kwa amani na heshima, akiitaka Serikali ya Burundi na ubalozi wake nchini Kenya kuwasaidia walioathirika.
Kidum aliwasihi Waburundi kutolipiza kisasi dhidi ya Wakenya walioko Burundi, akisema makosa mawili hayafanyi jambo kuwa sahihi. Pia aliitaka Tanzania kuwaacha Wakenya salama.
“Hili ni suala la kisiasa; litatatuliwa kisiasa,” alisema, akisisitiza diplomasia badala ya kulipiza kisasi.
Hata hivyo msanii huyo alishangaa iwapo ni makosa kufanya biashara ya kuuza chai, kahawa na mandazi.
Msemaji wa serikali Charles Owino tayari ametoa taarifa kuhusu suala hilo huku akionya raia wa Kenya dhidi ya kuwashambulia wageni.