Majeshi ya Yemen yashambulia waasi wa Houthi

Maafisa wanasema lengo ni kuutwaa tena mji mkuu, Sanaa, kutoka kwa kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.

Marion Bosire
2 Min Read

Wanajeshi waaminifu kwa serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa yameanzisha mashambulizi ya kulipiza dhidi ya waasi wa Houthi.

Maafisa wanasema wanalenga kuutwaa tena mji mkuu, Sanaa, kutoka kwa kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.

Mapigano yaliongezeka jana Jumatatu katika majimbo ya Taiz, al-Bayda na al-Jawf, yanayoonekana kuwa lango kuu kuelekea mji mkuu.

Majeshi ya serikali, yakisaidiwa na Saudi Arabia, yalisema yamefanya mashambulizi ya roketi na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya Houthi na kuripoti mapigano makali yaliyohusisha wanajeshi wa ardhini.

Waasi wa Houthi nao walisema wamezuia mashambulizi katika al-Jawf na kwamba angalau watu saba waliuawa katika shambulio la anga dhidi ya gereza katika mji wa al-Hazm.

Waliilaumu Riyadh kwa shambulio hilo, wakisema uchokozi huo hautaachwa bila adhabu.

Wakati huo huo, Saudi Arabia iliwashtumu Houthi kwa kuwajeruhi angalau raia 73, wakiwemo wanawake na watoto, katika mashambulizi ya hivi karibuni kwenye majimbo ya kusini mwa ufalme huo.

Riyadh pia iliahidi kuchukua hatua dhidi ya ongezeko hili hatari la mvutano.

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Yemen, Meja Jenerali Samir Al-Sabri, alisema katika taarifa iliyorushwa na televisheni ya taifa kwamba serikali imeamua “kuutwaa tena Sanaa”.

Majid al-Nuzaili, msemaji wa majeshi yanayotii serikali ya Yemen, alisema lengo la kampeni hiyo ni kuikomboa Yemen kutoka katika udhibiti wa Houthi na kurejesha Sanaa kuwa mji mkuu wa raia wote wa Yemen.

Raia nao wameonywa kuepuka barabara kadhaa kuu zinazoelekea Sanaa hasa njia zinazounganisha mji mkuu na Marib na al-Jawf, ikiwa ni pamoja na barabara zinazopita Nihm, Sirwah, Mahliyah na al-Hazm.

Share This Article