Rais William Ruto ametoa wito kwa makurutu wa polisi wa utawala waliofuzu leo Ijumaa kutumikia taifa kwa uadilifu na kuwajibikia vitendo vyao.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufuzu kwa makurutu hao huko Embakas jijini Nairobi, Ruto amewataka maafisa hao daima kukumbuka kuwa kiini cha mamlaka walio nayo ni katiba na hivyo wanapaswa wakati wote kujituma katika kutumikia raia.
Alisisitiza umuhimu wa mageuzi yanayoendelea katika idara ya polisi lakini akaongeza kuwa mageuzi hayo pasi ya huduma bora kwa raia hayana umuhimu wowote.
“Mwisho wa siku, kipimo kamili cha mageuzi ya polisi hakitapatikana katika hotuba, sera, vifaa, teknolojia au sare. Kitapatikana katika huduma zinazotolewa kwa raia,” alisema Rais Ruto.
“Kipimo cha kweli cha afisa si kile cha unachokifanya wakati taifa linakutazama, lakini kile unachokifanya wakati dhamiri yako, kiapo chako na sheria vinasimama kati ya kilicho sahihi na kilicho rahisi.”
Kiongozi wa nchi aliwasifia maafisa wa usalama kwa mchango wanaotoa kwa taifa akisema huwezesha sekta zote za nchi kuhudumu kwa manufaa ya nchi.
Hususan, aliwalimbikizia sifa polisi wa utawala akisema maafisa hao hushughulikia masuala magumu ya usalama wakati taifa linapowahitaji mno.
“Lazima tutambue mchango wa kila siku wa maafisa wa polisi. Wakati familia zinapolala, maafisa hukaa macho. Wakati hatari inapotokea, maafisa hujitokeza. Wakati jamii zinapotishiwa, maafisa husimama kati ya raia na madhara.”
Na huku akifahamu kuwa masuala kadhaa yameibuliwa kuhusiana na manunuzi ya sare mpya za polisi, Rais alielezea utayari wa utawala wake kuwajibikia matumizi ya fedha za umma ila bila kuchafuliana majina.
Kwa upande wake, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen aliwataka maafisa hao kuheshimu kiapo chao cha kutumikia taifa kwa uadilifu, akisema kufuzu kwao kutachangia kuboresha usalama wa nchi.
Alisema mtaala wa polisi umeboreshwa na kujumuishwa masuala kama vile haki za binadamu ili kuhakikisha utendaji kazi bora wa maafisa hao wanapokuwa kazini.