Busoga yaahirisha hafla kutoa heshima kwa Mfalme Oyo

Sherehe hizo za maadhimisho ya miaka 12 ya Mfalme Isebantu Kyabazinga William Wilberforce Gabula Nadiope IV, zitaandaliwa Jumamosi Septemba 19, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Ufalme wa kitamaduni wa Busoga nchini Uganda umetangaza kuahirishwa kwa hafla ya maadhimisho ya miaka 12 tangu aliposimikwa Mfalme Isebantu Kyabazinga William Wilberforce Gabula Nadiope IV.

Hatua hii inaripotiwa kuchochewa na haja ya kutoa heshima za Hayati Mfalme wa Ufalme wa Tooro nchini humo aliyeaga dunia akipokea matibabu nchini Marekani.

Waziri Mkuu wa ufalme wa Busoga, Dkt. Joseph Muvawala, alithibitisha kwamba uamuzi huo uliafikiwa kwa ajili ya kumuenzi Mfalme wa Tooro, Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV.

Sababu nyingine ya uamuzi huo, ni kuwapa raia wa Uganda wakiwemo wakazi wa Busoga fursa ya kuhudhuria mazishi ya Mfalme huyo ambayo tarehe yake inasadifiana na tarehe iliyokuwa imetengwa kwa maadhimisho ya Mfalme wa Busoga.

Sherehe hizo ambazo awali zilikuwa zimepangiwa kuandaliwa Septemba 13, 2026 sasa zitaandaliwa Jumamosi Septemba 19, 2026, kwenye uwanja wa makao makuu ya wilaya ya Mayuge.

Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV anatarajiwa kuzikwa Septemba 12, 2026, siku ya kumbukumbu ya miaka 31 tangu kutawazwa kwake kuwa Mfalme.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ameidhinisha mazishi rasmi yanayoungwa mkono na Serikali, huku bendera za taifa zikipeperushwa nusu mlingoti kwa siku tatu kama sehemu ya heshima kwa marehemu.

Mwili wa marehemu Mfalme Oyo unatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe kesho Ijumaa, Septemba 4, 2026, ambapo Rais Museveni anatarajiwa kuupokea.

Share This Article