Wadau wote muhimu kuhakikisha uchaguzi huru, asema Ethekon

Mwenyekiti huyo wa IEBC anasema watafanya kazi bega kwa bega na wadau wote ili kufanikisha uchaguzi mkuu ujao ulioratibiwa kufanywa Agosti 10, 2027.

Martin Mwanje
2 Min Read
Erastus Ethekon - Mwenyekiti wa IEBC

Wadau wote – wakiwemo Wakenya na taasisi mbalimbali – wana jukumu kubwa la kutekeleza kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027 ni huru na wa haki. 

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Erastus Ethekon anasema itakuwa vigumu kuitarajia tume hiyo kufanikisha uchaguzi huo kivyake.

“IEBC haiwezi ikaachiwa uchaguzi peke yake. Hiyo ndiyo sababu tulisema huru haimanishi haimanishi unafanyia kazi katika kisiwa fulani mahali fulani. Unafanyia kazi katika jamii ambayo ina washikadau tofauti na mbalimbali kabisa. Hiyo ndio sababu, kwangu, tangu nichukue wadhifa huu, niliuchukua mwanzo nikifahamu kwamba sitakuwa peke yangu,” alisema Ethekon.

“Naamini tuna kila sababu, tuna watu, tuna taasisi ambazo zitahakikisha uchaguzi unakuwa wa amani, wa kuaminika, huru na wa haki katika Jamhuri yetu.”

Mwenyekiti huyo aliyasema hayo wakati wa mkutano wa mashauriano kuhusu usalama wa kitaifa uliofanyika katika hoteli moja jijini Nairobi leo Jumatano.

Mkutano huo uliwaleta pamoja Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja, mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC Dkt. Kepha Wamae, na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou miongoni mwa wengine.

Kanja akitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wakenya kuzingatia amani kuelekea uchaguzi mkuu ujao, na kwamba maafisa wake watafanya kila wawezalo kuhakikisha Kenya inasalia salama.

“Hatuna nchi nyingine yoyote, hii ndio nchi yetu na tunaitaka kuwa ilivyo kabla, wakati na baada ya uchaguzi,” alisema Kanja katika wito ulioungwa mkono na Ethekon.

“Tutahakikisha uchaguzi ujao ni wa amani kwa kuongozwa na kanuni za kutoegemea upande wowote na kuzingatia utawala wa sheria.”

IEBC imetoa ratiba kamili kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 huku ikitenga Agosti 10 kuwa tarehe ambayo Wakenya wataelekea debeni kuwachagua viongozi wapya.

 

 

Share This Article