Visa vya maambukizi ya Ebola DRC vyafikia 6,100

Juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola zinaendelea nchini humo

Marion Bosire
2 Min Read

Visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola nchini DR Congo vimefikia 6,100, huku vifo kutokana na chamko hilo vikiwa takribani 2,950.

Juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola zinaendelea nchini humo na kwa mujibu wa taarifa ya hali ya ugonjwa iliyotolewa hivi karibuni, ugonjwa huo wa Ebola umeenea katika mikoa sita.

Maeneo 60 ya afya yameathirika bila kuripotiwa kwa eneo jipya kuathiriwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Ituri inaendelea kuwa kitovu kikuu cha maambukizi, ikiwa ndiyo Mkoa unaoongoza kwa idadi ya visa vilivyoripotiwa, takwimu zikionyesha kuwa hadi sasa watu 1,383 wamepona baada ya kupata matibabu, huku wagonjwa 814 wakiendelea kulazwa hospitalini au kutengwa kwa ajili ya ufuatiliaji na matibabu.

Katika juhudi za kupunguza maambukizi, wahudumu wa afya wameimarisha ufuatiliaji wa watu waliotagusana na wagonjwa.

Kiwango cha ufuatiliaji kimefikia asilimia 86.3, na kuvuka lengo la kiutendaji la asilimia 85 lililowekwa na mamlaka za afya.

Shughuli za kukabiliana na mlipuko huo zinajumuisha ufuatiliaji wa wagonjwa na watu waliokutana nao, matibabu, usafishaji na kuondoa virusi katika maeneo yaliyoathirika, pamoja na kampeni za kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Mamlaka za afya pia zimeendelea kutoa huduma za bila malipo za simu kupitia nambari 151, inayopatikana kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola au mtu mwenye dalili zinazohusishwa na ugonjwa huo.

Share This Article